Micah stands above lowland towns as overwhelming light breaks through storm clouds and water streams down mountains toward Samaria and Jerusalem

Mika 1

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Mika Mmoreshethi wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu.
2Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote, sikilizeni, ee dunia na wote mliomo, ili Bwana Mungu Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu, Bwana kutoka Hekalu lake takatifu.
3Tazama! Mwenyezi Mungu anakuja kutoka mahali pake; anashuka na kukanyaga mahali palipoinuka juu pa dunia.
4Milima inayeyuka chini yake na mabonde yanagawanyika kama nta mbele ya moto, kama maji yanayotiririka kasi kwenye mteremko.
5Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo, ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli. Kosa la Yakobo ni lipi? Je, sio Samaria? Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia ni nini? Je, sio Yerusalemu?
6“Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto, mahali pa kuotesha mizabibu. Nitayamwaga mawe yake katika bonde na kuacha wazi misingi yake.
7Sanamu zake zote zitavunjwa vipande vipande; zawadi zake zote za Hekalu zitachomwa kwa moto; nitaharibu vinyago vyake vyote. Kwa kuwa alikusanya zawadi zake kutokana na ujira wa kahaba, nazo zitatumika tena kulipa mishahara ya kahaba.”
8Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza; nitatembea bila viatu na tena uchi. Nitabweka kama mbweha na kuomboleza kama bundi.
9Kwa sababu jeraha lake halitibiki; limekuja kwa Yuda. Limefika hasa kwenye lango la watu wangu, hata Yerusalemu kwenyewe.
10Usiliseme hili huko Gathi; usilie hata kidogo. Huko Beth-le-Afra gaagaa mavumbini.
11Piteni mkiwa uchi na wenye aibu, ninyi mnaoishi Shafiri. Wale wanaoishi Saanani hawatatoka nje. Beth-Eseli iko katika maombolezo; kinga yake imeondolewa kwako.
12Wale wanaoishi Marothi wanagaagaa kwa maumivu wakingoja msaada, kwa sababu maangamizi yamekuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hata katika lango la Yerusalemu.
13Enyi mnaoishi Lakishi, fungeni farasi kwenye magari ya vita. Mlikuwa chanzo cha dhambi kwa Binti Sayuni, kwa kuwa makosa ya Israeli yalikutwa kwako.
14Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi zawadi za kuagana. Mji wa Akzibu utaonesha wazi udanganyifu kwa wafalme wa Israeli.
15Nitawaleteeni atakayewashinda ninyi mnaoishi Maresha. Yeye aliye utukufu wa Israeli atakuja Adulamu.
16Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia; jifanyieni upara kama tai, kwa kuwa watawaacha na kwenda uhamishoni.
‹ Yona 4Mika 2 ›

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.