
Mika 2
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ole kwa wale wapangao uovu, kwa wale wapangao hila vitandani mwao! Kunapopambazuka wanalitimiza kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.
2Wanatamani mashamba na kuyakamata, pia nyumba na kuzichukua. Wanamlaghai mwanaume nyumba yake, mwanadamu mwenzake urithi wake.
3Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu asema: “Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa, ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe. Hamtatembea tena kwa majivuno, kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa.
4Siku hiyo watu watawadhihaki, watawafanyia mzaha kwa wimbo huu wa maombolezo: ‘Tumeangamizwa kabisa; mali ya watu wangu imegawanywa. Ameninyang’anya! Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ”
5Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu wa kugawanya mashamba kwa kura.
6Manabii wao husema, “Usitabiri. Usitabiri kuhusu vitu hivi; aibu haitatupata.”
7Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo: “Je, Roho wa Mwenyezi Mungu amekasirika? Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?” “Je, maneno yangu hayamfanyii mema yeye ambaye njia zake ni nyofu?
8Siku hizi watu wangu wameinuka kama adui. Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita pasipo kujali, kama watu warudio kutoka vitani.
9Unawahamisha wanawake wa watu wangu kutoka nyumba zao za kupendeza. Unaondoa baraka yangu kwa watoto wao milele.
10Inuka, nenda zako! Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia, kwa sababu pametiwa unajisi, pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena.
11Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema, ‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’ angekuwa ndiye nabii anayekubalika na watu hawa!
12“Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo, Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli. Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi, kama kundi kwenye malisho yake, mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu.
13Yeye afunguaye njia atawatangulia; watapita kwenye lango na kutoka nje. Mfalme wao atawatangulia, Mwenyezi Mungu atakuwa kiongozi.”
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.