
Isaya 17
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Neno la unabii kuhusu Dameski: “Tazama, Dameski haitakuwa tena mji bali itakuwa lundo la magofu.
2Miji ya Aroeri itaachwa na itaachiwa mifugo ambayo italala huko, bila yeyote wa kuyaogopesha.
3Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu, nao uweza wa ufalme kutoka Dameski; mabaki ya Aramu yatakuwa kama utukufu wa Waisraeli,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
4“Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia, unono wa mwili wake utadhoofika.
5Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka na kuvuna nafaka kwa mikono yake, kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke katika Bonde la Warefai.
6Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki, kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa, kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi kileleni, nne au tano katika matawi yanayozaa sana,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli.
7Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa yule Aliye Mtakatifu wa Israeli.
8Hawataziangalia tena madhabahu, kazi za mikono yao, nao hawataheshimu nguzo za Ashera, na madhabahu za kufukizia uvumba zilizofanywa kwa mikono yao.
9Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.
10Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu, hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu. Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana na kuotesha mizabibu ya kigeni,
11hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote na asubuhi ile ile unayoipanda, unaifanya ichipue, hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu katika siku ile ya ugonjwa na maumivu yasiyoponyeka.
12Ole! Ghadhabu ya mataifa mengi: wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka! Ole! Makelele ya mataifa wanaovuma: wanavuma kama ngurumo za maji mengi!
13Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo za maji yanayofanya mawimbi, wakati anayakemea yanakimbia mbali, yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima, kama jani likivingirishwa na dhoruba.
14Wakati wa jioni, hofu ya ghafula! Kabla ya asubuhi, wametoweka! Hili ndilo fungu la wale wanaotupora, fungu la wale wanaotunyang’anya mali yetu.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.