Moabite envoys bringing lambs as refugees receive shelter before a just ruler seated near Jerusalem

Isaya 16

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Pelekeni wana-kondoo kama ushuru kwa mtawala wa nchi, Kutoka Sela, kupitia jangwani, hadi mlima wa Binti Sayuni.
2Kama ndege wanaopapatika waliofukuzwa kutoka kiota, ndivyo walivyo wanawake wa Moabu kwenye vivuko vya Mto Arnoni.
3“Tupeni shauri, toeni uamuzi. Wakati wa adhuhuri, fanyeni kivuli chenu kama usiku. Waficheni watoro, msisaliti wakimbizi.
4Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi; kuweni mahali pao pa salama ili kuepuka mwangamizi.” Mtesi atafikia mwisho na maangamizi yatakoma, aletaye vita atatoweka kutoka nchi.
5Kwa upendo kiti cha utawala kitaimarishwa, kwa uaminifu mtu ataketi juu yake, yeye atokaye nyumba ya Daudi: yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki, na huhimiza njia ya haki.
6Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu: kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu, kiburi chake na ufidhuli wake, lakini majivuno yake si kitu.
7Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza, wanaiombolezea Moabu kwa pamoja. Wanaomboleza na kuhuzunika kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi.
8Mashamba ya Heshboni yananyauka, pia na mizabibu ya Sibma. Watawala wa mataifa wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana, ambayo ilipata kufika Yazeri na kuenea kuelekea jangwani. Machipukizi yake yalienea yakafika hadi baharini.
9Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo, kwa ajili ya mizabibu ya Sibma. Ee Heshboni, ee Eleale, ninakulowesha kwa machozi! Shangwe za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa.
10Furaha na shangwe zimeondolewa kutoka mashamba ya matunda; hakuna yeyote aimbaye wala apazaye sauti katika mashamba ya mizabibu; hakuna yeyote akanyagaye zabibu shinikizoni, kwa kuwa nimekomesha makelele.
11Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi, nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi.
12Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu pa kuabudia, anajichosha mwenyewe tu; anapoenda mahali pake pa ibada za sanamu ili kuomba, haitamfaidi lolote.
13Hili ndilo neno ambalo Mwenyezi Mungu ameshasema kuhusu Moabu.
14Lakini sasa Mwenyezi Mungu anasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana, tena wanyonge.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.