Cushite envoys traveling in reed boats toward a distant mountain marked by a raised signal banner

Isaya 18

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa , kando ya mito ya Kushi,
2iwapelekayo wajumbe wake kupitia bahari kwa mashua za mafunjo juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito.
3Enyi mataifa yote ya ulimwengu, ninyi mnaoishi duniani wakati bendera itakapoinuliwa milimani, mtaiona, nayo tarumbeta itakapolia, mtaisikia.
4Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nitatulia kimya na kutazama kutoka maskani yangu, kama joto linalometameta katika mwanga wa jua, kama wingu la umande katika joto la wakati wa mavuno.”
5Kwa maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua ukishapita na maua yakawa zabibu zinazoiva, atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi, naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka.
6Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani na wanyama pori, ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi, nao wanyama pori wakati wote wa masika.
7Wakati huo matoleo yataletwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito, matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.