Families, children, elders, and shepherds celebrate before restored Jerusalem while people from many nations approach open gates beneath radiant dawn

Sefania 3

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ole mji wa wadhalimu, waasi na waliotiwa unajisi!
2Hautii mtu yeyote, haukubali maonyo. Haumtumaini Mwenyezi Mungu, haukaribii karibu na Mungu wake.
3Maafisa wake ni simba wanaonguruma, watawala wake ni mbwa-mwitu wa jioni, ambao hawabakizi chochote kwa ajili ya asubuhi.
4Manabii wake ni wenye kiburi, ni wadanganyifu. Makuhani wake hunajisi patakatifu na kuihalifu sheria.
5Mwenyezi Mungu aliye ndani yake ni mwenye haki, hafanyi kosa. Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake, kila kukipambazuka huitimiza, bali mtu dhalimu hana aibu.
6“Nimeyaangamiza mataifa, ngome zao zimebomolewa. Nimeziacha barabara ukiwa, hakuna anayepita humo. Miji yao imeharibiwa; hakuna mmoja atakayeachwa: hakuna hata mmoja.
7Niliuambia huo mji, ‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’ Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali, wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake. Lakini walikuwa bado na shauku kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
8Mwenyezi Mungu anasema, “Kwa hiyo ningojee mimi, siku nitakayosimama kuteka nyara. Nimeamua kukusanya mataifa, kukusanya falme na kumimina ghadhabu yangu juu yao, hasira yangu kali yote. Dunia yote itateketezwa kwa moto wa hasira yangu yenye wivu.
9“Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa, kwamba wote waweze kuliitia jina la Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa pamoja.
10Kutoka ng’ambo ya mito ya Kushi watu wangu wanaoniabudu, watu wangu waliotawanyika, wataniletea sadaka.
11Siku hiyo hutaaibishwa kwa ajili ya makosa yote uliyonitendea, kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu wale wote wanaoshangilia katika kiburi chao. Kamwe hutajivuna tena katika kilima changu kitakatifu.
12Lakini nitakuachia ndani yako wapole na wanyenyekevu, ambao wanatumaini jina la Mwenyezi Mungu.
13Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa; hawatasema uongo, wala udanganyifu hautakuwa katika vinywa vyao. Watakula na kulala wala hakuna yeyote atakayewaogopesha.”
14Imba, ee Binti Sayuni; paza sauti, ee Israeli! Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee Binti Yerusalemu!
15Mwenyezi Mungu amekuondolea adhabu yako, amewarudisha nyuma adui zako. Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe; kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
16Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu, “Usiogope, ee Sayuni; usiiache mikono yako ilegee.
17Mwenyezi Mungu, Mungu wako, yu pamoja nawe, yeye ni Shujaa mwenye nguvu anayeokoa. Atakufurahia kwa furaha kubwa, atakutuliza kwa pendo lake, atakufurahia kwa kuimba.”
18“Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa nitaziondoa kwenu; hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
19Wakati huo nitawaadhibu wote waliokudhulumu; nitaokoa vilema na kukusanya wale waliotawanywa. Nitawapa sifa na heshima katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
20Wakati huo nitawakusanya; wakati huo nitawaleta nyumbani. Nitawapa sifa na heshima miongoni mwa mataifa yote ya dunia wakati nitakapowarudishia mateka yenu mbele ya macho yenu hasa,” asema Mwenyezi Mungu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.