A humble community gathers around Zephaniah on a green rise between ruined coasts, salt wastes, arid lands, and abandoned Assyrian towers

Sefania 2

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja, enyi taifa lisilo na aibu,
2kabla wakati ulioamriwa haujafika na siku ile inayopeperusha kama makapi, kabla hasira kali ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu, kabla siku ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu.
3Mtafuteni Mwenyezi Mungu, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi, ninyi ambao hufanya lile analoamuru. Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu; labda mtahifadhiwa siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu.
4Gaza utaachwa na Ashkeloni utaachwa magofu. Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu, na Ekroni utang’olewa.
5Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari, enyi Wakerethi; neno la Mwenyezi Mungu liko dhidi yenu, ee Kanaani, nchi ya Wafilisti. “Mimi nitawaangamiza, na hakuna atakayebaki.”
6Nchi iliyo karibu na bahari itakuwa malisho yenye visima vya wachungaji, na mazizi ya kondoo.
7Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda, hapo watapata malisho. Wakati wa jioni watajilaza chini katika nyumba za Ashkeloni. Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawatunza, naye atawarudishia wafungwa wao.
8“Nimeyasikia matukano ya Moabu nazo dhihaka za Waamoni, ambao waliwatukana watu wangu na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.
9Hakika, kama niishivyo,” asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, “hakika Moabu itakuwa kama Sodoma, Waamoni kama Gomora: mahali pa magugu na mashimo ya chumvi, nchi ya ukiwa milele. Mabaki ya watu wangu watawateka nyara; mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”
10Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao, kwa kutukana na kudhihaki watu wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
11Mwenyezi Mungu atakuwa wa kuhofisha kwao atakapoangamiza miungu yote ya nchi. Mataifa katika kila pwani yatamwabudu, kila moja katika nchi yake.
12“Ninyi pia, ee Wakushi, mtauawa kwa upanga wangu.”
13Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini na kuangamiza Waashuru, akiiacha Ninawi ukiwa na pakame kama jangwa.
14Makundi ya kondoo na ng’ombe yatajilaza pale, viumbe vya kila aina. Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba wataishi juu ya nguzo zake. Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani, kifusi kitakuwa milangoni, boriti za mwerezi zitaachwa wazi.
15Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha wakijisikia salama. Ulisema moyoni mwako, “Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.” Jinsi gani umekuwa gofu, mahali pa kulala wanyama pori! Wote wanaopita kando yake wanauzomea na kutikisa mkono kwa dharau.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.