A pilgrim family drinks at a hillside spring as swallows nest and musicians welcome them near Jerusalem

Zaburi 84

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, makao yako yapendeza kama nini!
2Nafsi yangu inatamani sana, naam, hata kuona shauku, kwa ajili ya nyua za Mwenyezi Mungu; moyo wangu na mwili wangu vinamlilia Mungu Aliye Hai.
3Hata shomoro amejipatia makao, mbayuwayu amejipatia kiota mahali awezapo kuweka makinda yake: mahali karibu na madhabahu yako, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mfalme wangu na Mungu wangu.
4Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wanaokusifu wewe daima.
5Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako, na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
6Wanapopita katika Bonde la Baka , hulifanya mahali pa chemchemi, pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi .
7Huendelea toka nguvu hadi nguvu, hadi kila mmoja afikapo mbele za Mungu huko Sayuni.
8Ee Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, sikia maombi yangu; nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
9Ee Mungu, uitazame ngao yetu, mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
10Siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
11Kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu ni jua na ngao; Mwenyezi Mungu hutoa wema na heshima; hakuna kitu chema anachowanyima wale ambao hawana hatia.
12Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, heri mtu anayekutumaini wewe.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.