
Zaburi 48
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Mwenyezi Mungu ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu, mlima wake mtakatifu.
2Ni mzuri katika kuinuka juu kwake, furaha ya dunia yote. Kama vilele vya juu vya Safoni ni Mlima Sayuni, mji wa Mfalme Mkuu.
3Mungu yuko katika ngome zake; amejionesha mwenyewe kuwa ngome yake.
4Wafalme walipounganisha nguvu, waliposonga mbele pamoja,
5walimwona, wakashangaa, wakakimbia kwa hofu.
6Kutetemeka kuliwashika huko, maumivu kama ya mwanamke mwenye uchungu wa kuzaa.
7Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi zilizovunjwa na upepo wa mashariki.
8Kama tulivyokuwa tumesikia, ndivyo tulivyoona katika mji wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, katika mji wa Mungu wetu: Mungu ataufanya uwe salama milele.
9Ee Mungu, hekaluni mwako tunatafakari upendo wako usiokoma.
10Ee Mungu, kama jina lako lilivyo, sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia, mkono wako wa kuume umejazwa na haki.
11Mlima Sayuni unashangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako.
12Tembeeni katika Sayuni, uzungukeni mji, hesabuni minara yake;
13yatafakarini vyema maboma yake, angalieni ngome zake, ili mpate kusimulia habari zake kwa kizazi kijacho.
14Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.