
Zaburi 32
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Heri mtu aliyesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimefunikwa.
2Heri mtu yule ambaye Mwenyezi Mungu hamhesabii dhambi, na ambaye rohoni mwake hamna udanganyifu.
3Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
4Usiku na mchana mkono wako ulinilemea, nguvu zangu zilinyonywa kama vile katika joto la kiangazi.
5Kisha nikakiri dhambi yangu kwako, wala sikuficha uovu wangu. Nilisema, “Nitaungama makosa yangu kwa Mwenyezi Mungu.” Ndipo uliponisamehe hatia ya dhambi yangu.
6Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe wakati unapopatikana, hakika maji makuu yatakapofurika hayatamfikia yeye.
7Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha, utaniepusha na taabu na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
8Nitakufundisha na kukuonesha njia utakayoiendea; nitakushauri na kukuangalia.
9Usiwe kama farasi au nyumbu wasio na akili, ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu la sivyo hawatakukaribia.
10Mtu mwovu ana taabu nyingi, bali upendo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu unamzunguka mtu anayemtumaini.
11Shangilieni katika Mwenyezi Mungu na mfurahi, enyi wenye haki! Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.