A besieged man prays above enemies and broken nets as friends welcome him into safety

Zaburi 31

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mwenyezi Mungu, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe, kwa haki yako uniokoe.
2Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka; uwe kwangu mwamba wa kimbilio, ngome imara ya kuniokoa.
3Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu, uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako.
4Uniepushe na mtego niliotegewa, maana wewe ndiwe kimbilio langu.
5Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako, unikomboe Ee Mwenyezi Mungu, uliye Mungu wa kweli.
6Ninawachukia wale wanaoshikilia sanamu batili; bali mimi ninamtumaini Mwenyezi Mungu.
7Nitafurahia na kushangilia upendo wako, kwa kuwa uliona mateso yangu na ulijua maumivu ya nafsi yangu.
8Hukunikabidhi kwa adui yangu bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi.
9Ee Mwenyezi Mungu unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida; macho yangu yanafifia kwa huzuni, nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.
10Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi, naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali; nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso, na mifupa yangu inachakaa.
11Kwa sababu ya adui zangu wote, nimedharauliwa kabisa na majirani zangu, hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho, wale wanaoniona barabarani wananikimbia.
12Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa, nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.
13Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi; vitisho viko pande zote; kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu, na kula njama kuniua.
14Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Mwenyezi Mungu; nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
15Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako, uniokoe mikononi mwa adui zangu na wale wanifuatiao.
16Mwangazie mtumishi wako uso wako, uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.
17Usiniache niaibike, Ee Mwenyezi Mungu, kwa maana nimekulilia wewe, bali waovu waaibishwe na kunyamazishwa Kuzimu.
18Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe, kwa maana kwa kiburi na dharau wao husema kwa majivuno dhidi ya wenye haki.
19Tazama jinsi wema wako ulivyo mkuu, uliowawekea akiba wanaokucha, unaowapa wale wanaokukimbilia machoni pa watu wote.
20Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako kutokana na hila za wanadamu; katika makao yako huwaweka salama kutokana na ndimi za mashtaka.
21Atukuzwe Mwenyezi Mungu, kwa kuwa amenionesha upendo wake wa ajabu nilipokuwa katika mji uliozingirwa.
22Katika hofu yangu nilisema, “Nimekatiliwa mbali na macho yako!” Hata hivyo ulisikia kilio changu ukanihurumia nilipokuita unisaidie.
23Mpendeni Mwenyezi Mungu ninyi watakatifu wake wote! Mwenyezi Mungu huwahifadhi waaminifu, lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.
24Kuweni hodari na mjipe moyo, ninyi nyote mnaomtumaini Mwenyezi Mungu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.