A kneeling psalmist prays by a stone wall as a shepherd leader and musicians gather nearby

Zaburi 28

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ninakuita wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mwamba wangu; usikatae kunisikiliza. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni.
2Sikia kilio changu nikikuomba unihurumie, ninapokuita ili unisaidie, ninapoinua mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako.
3Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na majirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki.
4Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili.
5Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Mwenyezi Mungu, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena.
6Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie.
7Mwenyezi Mungu ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo.
8Mwenyezi Mungu ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake.
9Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.