
Zaburi 27
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Mwenyezi Mungu ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Mwenyezi Mungu ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani?
2Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wale nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka.
3Hata jeshi linizingire pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri.
4Jambo moja ninamwomba Mwenyezi Mungu, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Mwenyezi Mungu na kumtafuta hekaluni mwake.
5Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema lake, na kuniweka juu kwenye mwamba.
6Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia Mwenyezi Mungu na kumsifu.
7Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Mwenyezi Mungu, unihurumie na unijibu.
8Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, Mwenyezi Mungu “Nitautafuta.”
9Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu.
10Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, Mwenyezi Mungu atanipokea.
11Nifundishe njia yako, Ee Mwenyezi Mungu, niongoze katika njia iliyo nyoofu, kwa sababu ya watesi wangu.
12Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri.
13Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa Mwenyezi Mungu katika nchi ya walio hai.
14Mngojee Mwenyezi Mungu; uwe hodari na mwenye moyo mkuu, na umngojee Mwenyezi Mungu.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.