
Zaburi 21
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mwenyezi Mungu, mfalme huzifurahia nguvu zako. Tazama jinsi furaha yake ilivyo kuu kwa ushindi unaompa!
2Umempa haja ya moyo wake na hukumzuilia maombi ya midomo yake.
3Ulimkaribisha kwa baraka tele na kumvika taji la dhahabu safi kichwani pake.
4Alikuomba maisha, nawe ukampa, wingi wa siku milele na milele.
5Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa, umeweka juu yake fahari na utukufu.
6Hakika umempa baraka za milele, umemfanya awe na furaha kwa shangwe ya uwepo wako.
7Kwa kuwa mfalme anamtumaini Mwenyezi Mungu; kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa.
8Mkono wako utawashika adui zako wote, mkono wako wa kuume utawakamata adui zako.
9Wakati utajitokeza, utawafanya kama tanuru la moto. Katika ghadhabu yake Mwenyezi Mungu atawameza, moto wake utawateketeza.
10Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani, uzao wao kutoka wanadamu.
11Ingawa watapanga mabaya dhidi yako na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa,
12kwa kuwa utawafanya wakimbie utakapowalenga usoni pao kwa mshale kutoka upinde wako.
13Ee Mwenyezi Mungu, utukuzwe katika nguvu zako, tutaimba na kusifu nguvu zako.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.