A royal bier departs while prisoners are freed and widows, immigrants, hungry families, and blind elders receive help

Zaburi 146

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Msifuni Mwenyezi Mungu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi Mungu,
2Nitamsifu Mwenyezi Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu sifa wakati wote ningali hai.
3Usiweke tumaini lako kwa wakuu, kwa wanadamu ambao hufa, ambao hawawezi kuokoa.
4Roho yao itokapo hurudi mavumbini, siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma.
5Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, ambaye tumaini lake ni katika Mwenyezi Mungu, Mungu wake,
6Muumba wa mbingu na nchi, na bahari na vyote vilivyomo: Mwenyezi Mungu anayedumu kuwa mwaminifu milele na milele.
7Naye huwapatia haki waliodhulumiwa, na kuwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi Mungu huwaweka wafungwa huru,
8Mwenyezi Mungu huwafumbua vipofu macho, Mwenyezi Mungu huwainua waliolemewa na mizigo yao, Mwenyezi Mungu huwapenda wenye haki.
9Mwenyezi Mungu huwalinda wageni na kuwategemeza yatima na wajane, lakini hupinga njia za waovu.
10Mwenyezi Mungu atamiliki milele, Mungu wako, ee Sayuni, kwa vizazi vyote. Msifuni Mwenyezi Mungu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.