
Mika 5
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi, kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu. Watampiga mtawala wa Israeli shavuni kwa fimbo.
2“Lakini wewe, Bethlehemu Efrata, ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda, kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli, ambaye asili yake ni kutoka zamani, kutoka milele.”
3Kwa hiyo Israeli utaachwa hadi mwanamke aliye na uchungu atakapozaa mwana, na ndugu zake wengine warudi kujiunga na Waisraeli.
4Atasimama na kulichunga kundi lake katika nguvu ya Mwenyezi Mungu, katika utukufu wa jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake. Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.
5Naye atakuwa amani yao. Ukombozi na uharibifu Mwashuru atakapovamia nchi yetu na kupita katika ngome zetu, tutawainua wachungaji saba dhidi yake, hata viongozi wanane wa watu.
6Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga, nchi ya Nimrodi kwa upanga. Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru atakapoivamia nchi yetu na kuingia katika mipaka yetu.
7Mabaki ya Yakobo yatakuwa katikati ya mataifa mengi kama umande kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama manyunyu juu ya majani, ambayo hayamngoji mtu wala kukawia kwa mwanadamu.
8Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa, katikati ya mataifa mengi, kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni, kama mwana simba miongoni mwa makundi ya kondoo, ambaye anaumiza vibaya na kuwararua kila anapopita katikati yao, wala hakuna awezaye kuokoa.
9Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako, nao adui zako wote wataangamizwa.
10“Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu, “nitaangamiza farasi wenu kati yenu, na kubomoa magari yenu ya vita.
11Nitaiangamiza miji ya nchi yenu, na kuziangusha chini ngome zenu zote.
12Nitaangamiza uchawi wenu, na hamtapiga tena ramli.
13Nitaangamiza sanamu zenu, na mawe yenu ya ibada yatoke kati yenu; hamtasujudia tena kazi ya mikono yenu.
14Nitang’oa nguzo za Ashera kati yenu, na kubomoa miji yenu.
15Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu, kwa mataifa ambayo hayajanitii.”
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.