Priests, rulers, and people stand trapped behind a hunter's net as a lion's shadow looms over the road ahead

Hosea 5

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1“Sikieni hili, enyi makuhani! Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli! Sikieni, ee nyumba ya mfalme! Hukumu hii ni dhidi yenu: Mmekuwa mtego huko Mispa, wavu uliotandwa juu ya Tabori.
2Waasi wamezidisha sana mauaji. Mimi nitawatiisha wote.
3Ninajua yote kuhusu Efraimu, Israeli hukufichika kwangu. Efraimu, sasa umegeukia ukahaba, Israeli amenajisika.
4“Matendo yao hayawaachii kurudi kwa Mungu wao. Roho ya ukahaba iko ndani ya mioyo yao, hawamkubali Mwenyezi Mungu.
5Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao; Waisraeli, hata Efraimu, wanajikwaa katika dhambi zao; pia Yuda atajikwaa pamoja nao.
6Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ng’ombe kumtafuta Mwenyezi Mungu, hawatampata; yeye amejiondoa kutoka kwao.
7Wao si waaminifu kwa Mwenyezi Mungu; wamezaa watoto haramu. Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi zitawaangamiza wao pamoja na mashamba yao.
8“Pigeni tarumbeta huko Gibea, na baragumu huko Rama. Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni ; ongoza, ee Benyamini.
9Efraimu ataachwa ukiwa katika siku ya kuadhibiwa. Miongoni mwa makabila ya Israeli ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia.
10Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji.
11Efraimu amedhulumiwa, amekanyagwa katika hukumu kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu.
12Mimi ni kama nondo kwa Efraimu, na kama uozo kwa watu wa Yuda.
13“Efraimu alipoona ugonjwa wake, naye Yuda vidonda vyake, ndipo Efraimu aligeukia Ashuru, na kuomba msaada kwa mfalme mkuu. Lakini hawezi kukuponya, hawezi kukuponya vidonda vyako.
14Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu, kama simba mkubwa kwa Yuda. Nitawararua vipande vipande na kuondoka; nitawachukua mbali, na hakuna wa kuwaokoa.
15Kisha nitarudi mahali pangu hadi watakapokubali kosa lao. Nao watautafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.