Gaius welcoming dusty messengers with food and supplies beside a neighboring closed doorway

3 Yohana 1

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Mzee. Kwa Gayo rafiki yangu nimpendaye katika kweli.
2Mpendwa, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya njema kama vile roho yako ifanikiwavyo.
3Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza kuhusu uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli.
4Sina furaha kubwa kuliko hii, ya kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.
5Rafiki mpendwa, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako.
6Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya jumuiya ya waumini. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu.
7Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasiomwamini Al-Masihi.
8Kwa hiyo imetupasa sisi kuonesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.
9Nililiandikia kundi la waumini, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu.
10Hivyo nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu, na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke miongoni mwa waumini.
11Rafiki mpendwa, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Yeyote atendaye mema anatoka kwa Mungu, bali atendaye mabaya hajamwona Mungu.
12Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.
13Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino.
14Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.
15Amani iwe kwako. Rafiki zetu walio hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walio huko, kila mmoja kwa jina lake.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.