A couple reunited on a lamplit city street with a wedding procession in the distance

Wimbo Ulio Bora 3

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Usiku kucha kwenye kitanda changu nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye; nilimtafuta, lakini sikumpata.
2Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini, katika barabara zake na viwanja; nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye. Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata.
3Walinzi walinikuta walipokuwa wakizunguka mji. Nikawauliza, “Je, mmemwona yule moyo wangu umpendaye?”
4Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita nilimpata yule moyo wangu umpendaye. Nilimshika na sikumwachia aende hadi nilipomleta katika nyumba ya mama yangu, katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.
5Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe.
6Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani kama nguzo ya moshi, anayenukia manemane na uvumba iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote vya mfanyabiashara?
7Tazama! Ni gari la Sulemani likisindikizwa na mashujaa sitini, walio wakuu sana wa Israeli,
8wote wamevaa panga, wote wazoefu katika vita, kila mmoja na upanga wake pajani, wamejiandaa kwa ajili ya vitisho vya usiku.
9Mfalme Sulemani alijitengenezea gari; alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.
10Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha, kitako chake kwa dhahabu. Kiti chake kilipambwa kwa zambarau, gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo na binti za Yerusalemu.
11Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni, mkamtazame Mfalme Sulemani akiwa amevaa taji, taji ambalo mama yake alimvika siku ya arusi yake, siku ambayo moyo wake ulishangilia.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.