
Zaburi 79
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, wamelinajisi Hekalu lako takatifu, wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.
2Wametoa maiti za watumishi kuwa chakula cha ndege wa angani na nyama ya watakatifu wako kwa wanyama wa nchi.
3Wamemwaga damu kama maji kuzunguka Yerusalemu yote, wala hakuna yeyote wa kuwazika.
4Tumekuwa kitu cha aibu kwa majirani zetu, cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.
5Hata lini, Ee Mwenyezi Mungu? Je, wewe utakasirika milele? Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?
6Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,
7kwa maana wamemrarua Yakobo na kuharibu nchi ya makao yake.
8Usituhesabie dhambi za baba zetu, huruma yako na itujie hima, kwa maana tu wahitaji mno.
9Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako.
10Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wenu?” Mbele ya macho yetu, dhihirisha kati ya mataifa kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa ya watumishi wako.
11Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; kwa nguvu za mkono wako hifadhi wale waliohukumiwa kufa.
12Walipize majirani zetu mara saba aibu walizovurumisha kwako, Ee Bwana.
13Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; tutasimulia sifa zako kizazi hadi kizazi.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.