Worshipers gather near the sanctuary as rain revives fields, streams, grain, and grazing flocks

Zaburi 65

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa.
2Ewe usikiaye maombi, watu wote watakuja kwako wewe.
3Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, wewe ulisamehe makosa yetu.
4Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu.
5Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, Ee Mungu Mwokozi wetu, tumaini la miisho yote ya duniani na la bahari zilizo mbali sana,
6uliyeumba milima kwa uwezo wako, ukiwa umejivika nguvu,
7uliyenyamazisha dhoruba za bahari, ngurumo za mawimbi yake, na ghasia za mataifa.
8Wale wanaoishi mbali sana wanaogopa maajabu yako, kule asubuhi ipambazukiapo na kule jioni inakofifilia umeziita nyimbo za furaha.
9Waitunza nchi na kuinyeshea, waitajirisha kwa wingi. Vijito vya Mungu vimejaa maji ili kuwapa watu nafaka, kwa maana wewe umeviamuru.
10Umeilowesha mifereji yake na kusawazisha kingo zake; umeilainisha kwa manyunyu na kuibariki mimea yake.
11Umeuvika mwaka taji la baraka, magari yako yanafurika kwa wingi.
12Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; vilima vimevikwa furaha.
13Malisho yamejaa makundi ya wanyama, na mabonde yamepambwa kwa mavuno; vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.