A boastful official threatens a family while a faithful man stands beside a green olive tree

Zaburi 52

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya? Kwa nini unajivuna mchana kutwa, wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?
2Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi. Ni kama wembe mkali, ninyi mnaofanya hila.
3Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli.
4Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila!
5Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka hema lako, atakung’oa kutoka nchi ya walio hai.
6Wenye haki wataona na kuogopa; watamcheka, wakisema,
7“Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake, bali alitumainia wingi wa utajiri wake, na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”
8Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, nautegemea upendo wa Mungu usiokoma milele na milele.
9Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda, nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema. Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.