
Zaburi 38
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mwenyezi Mungu, usinikemee katika hasira yako, wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.
2Kwa kuwa mishale yako imenichoma, na mkono wako umenipiga.
3Hakuna afya mwilini mwangu kwa sababu ya ghadhabu yako, mifupa yangu haina uzima kwa sababu ya dhambi zangu.
4Maovu yangu yamenifunika kama mzigo mzito mno.
5Majeraha yangu yameoza na yananuka, kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
6Nimeinamishwa chini na kushushwa sana, mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.
7Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo, hakuna afya mwilini mwangu.
8Nimedhoofika na kupondwa kabisa, nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.
9Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku yako wazi mbele zako, kutamani kwangu sana hakufichiki mbele zako.
10Moyo wangu unapigapiga, nguvu zangu zimeniishia; hata macho yangu yametiwa giza.
11Rafiki na wenzangu wananikwepa kwa sababu ya majeraha yangu; majirani wangu wanakaa mbali nami.
12Wale wanaotafuta uhai wangu wanatega mitego yao, wale ambao wangetaka kunidhuru huongea kuhusu maangamizi yangu; hupanga hila mchana kutwa.
13Mimi ni kama kiziwi, asiyeweza kusikia, ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake;
14nimekuwa kama mtu asiyesikia, ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.
15Ee Mwenyezi Mungu, ninakungojea wewe, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, utajibu.
16Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie, wala wajitukuze juu yangu mguu wangu unapoteleza.”
17Kwa maana ninakaribia kuanguka, na maumivu yangu yananiandama siku zote.
18Naungama uovu wangu, ninataabishwa na dhambi yangu.
19Wengi wamekua adui zangu bila sababu; wale wanaonichukia bure ni wengi.
20Wanaolipa wema wangu kwa maovu hunisingizia ninapofuata lililo jema.
21Ee Mwenyezi Mungu, usiniache, usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.
22Ee Bwana Mwokozi wangu, uje upesi kunisaidia.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.