A fugitive gathers poor and fearful people around bread as danger recedes at sunrise

Zaburi 34

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Nitamtukuza Mwenyezi Mungu nyakati zote, sifa zake zitakuwa mdomoni mwangu siku zote.
2Nafsi yangu itajisifu katika Mwenyezi Mungu, walioonewa watasikia na wafurahi.
3Mtukuzeni Mwenyezi Mungu pamoja nami, naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
4Nilimtafuta Mwenyezi Mungu naye akanijibu, akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
5Wale wamtazamao hutiwa nuru, nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
6Maskini huyu alimwita Mwenyezi Mungu, naye akamsikia, akamwokoa katika taabu zake zote.
7Malaika wa Mwenyezi Mungu hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa.
8Onjeni mwone kwamba Mwenyezi Mungu ni mwema; heri mtu yule anayemkimbilia.
9Mcheni Mwenyezi Mungu enyi watakatifu wake, kwa maana wale wamchao hawapungukiwi na chochote.
10Wana simba wenye nguvu hutindikiwa na kuona njaa, bali wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
11Njooni, watoto wangu, mnisikilize, nitawafundisha kumcha Mwenyezi Mungu.
12Yeyote kati yenu anayependa uzima na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo.
14Aache uovu, atende mema, aitafute amani na kuifuatilia.
15Macho ya Mwenyezi Mungu huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
16Uso wa Mwenyezi Mungu uko kinyume na watendao maovu, ili kufuta kumbukumbu lao duniani.
17Wenye haki hulia, naye Mwenyezi Mungu huwasikia, huwaokoa katika taabu zao zote.
18Mwenyezi Mungu yu karibu na waliovunjika moyo, na huwaokoa waliopondeka roho.
19Mwenye haki ana mateso mengi, lakini Mwenyezi Mungu humwokoa nayo yote,
20huhifadhi mifupa yake yote, hata mmoja hautavunjika.
21Ubaya utamuua mtu mwovu, nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
22Mwenyezi Mungu huwakomboa watumishi wake, yeyote anayemkimbilia yeye hatahukumiwa kamwe.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.