
Zaburi 17
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Sikia, Ee Mwenyezi Mungu, kusihi kwangu kwa haki, sikiliza kilio changu. Tega sikio kwa ombi langu, halitoki katika midomo ya udanganyifu.
2Hukumu yangu na itoke kwako, macho yako na yaone yale yaliyo haki.
3Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku, ingawa umenijaribu, hutaona chochote. Nimeamua kwamba kinywa changu hakitatenda dhambi.
4Kuhusu matendo ya wanadamu: kwa neno la midomo yako, nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
5Hatua zangu zimeshikamana na njia zako; nyayo zangu hazikuteleza.
6Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu, nitegee sikio lako na usikie ombi langu.
7Uoneshe ajabu ya upendo wako mkuu, wewe unayeokoa kwa mkono wako wa kuume wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.
8Nilinde kama mboni ya jicho lako, unifiche chini ya kivuli cha mabawa yako
9kutokana na waovu wanaonishambulia, kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.
10Huifunga mioyo yao iliyo migumu, vinywa vyao hunena kwa majivuno.
11Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira, wakiwa macho, waniangushe chini.
12Wamefanana na simba mwenye njaa anayewinda, kama simba mkubwa anayenyemelea mafichoni.
13Inuka, Ee Mwenyezi Mungu, pambana nao, uwaangushe, niokoe kwa upanga wako kutoka kwa waovu.
14Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako uniokoe na watu kama hawa, kutokana na watu wa ulimwengu huu ambao fungu lao liko katika maisha haya. Na wapate adhabu ya kuwatosha. Watoto wao na wapate zaidi ya hayo, hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao.
15Bali mimi nitauona uso wako katika haki; niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.