A man prays beside evening incense while touching his mouth and avoiding a corrupt feast

Zaburi 141

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Ee Mwenyezi Mungu, ninakuita, njoo kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita.
2Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.
3Ee Mwenyezi Mungu, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
4Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
5Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda maovu.
6Watawala wao watatupwa chini kutoka majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli.
7Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”
8Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.
9Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda maovu.
10Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.