Friends pull a grateful man from a ravine as he carries a cup toward gathered sanctuary worshipers

Zaburi 116

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Nampenda Mwenyezi Mungu kwa maana amesikia sauti yangu; amesikia kilio changu ili anihurumie.
2Kwa sababu amenitegea sikio lake, nitamwita siku zote za maisha yangu.
3Kamba za mauti zilinizunguka, vitisho vya Kuzimu vilinipata, nikalemewa na taabu na huzuni.
4Ndipo nikaliitia jina la Mwenyezi Mungu: “Ee Mwenyezi Mungu, niokoe!”
5Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na haki, Mungu wetu ni mwingi wa huruma.
6Mwenyezi Mungu huwalinda wanyenyekevu, nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.
7Ee nafsi yangu, tulia tena, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuwa mwema kwako.
8Kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umeniokoa nafsi yangu na mauti, macho yangu kutokana na machozi, miguu yangu kutokana na kujikwaa,
9ili niweze kutembea mbele za Mwenyezi Mungu, katika nchi ya walio hai.
10Nilimwamini Mwenyezi Mungu, niliposema, “Mimi nimeteseka sana.”
11Katika taabu yangu nilisema, “Wanadamu wote ni waongo.”
12Nimrudishie Mwenyezi Mungu nini kwa wema wake wote alionitendea?
13Nitakiinua kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu.
14Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu mbele za watu wake wote.
15Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa Mwenyezi Mungu.
16Ee Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mtumishi wako, mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako ; umeniweka huru toka katika minyororo yangu.
17Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru na kuliita jina la Mwenyezi Mungu.
18Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu mbele za watu wake wote,
19katika nyua za nyumba ya Mwenyezi Mungu, katikati yako, ee Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi Mungu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.