
Zaburi 11
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Kwa Mwenyezi Mungu ninakimbilia. Unawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege utorokee kwenye mlima wako.
2Hebu tazama, waovu wanapinda nyuta zao; wanaweka mishale kwenye nyuzi zake ili wakiwa gizani, wawapige walio wanyofu wa moyo.
3Wakati misingi imeharibiwa, mwenye haki anaweza kufanya nini?”
4Mwenyezi Mungu yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; Mwenyezi Mungu yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawachunguza.
5Mwenyezi Mungu huwachunguza wenye haki, lakini nafsi yake inachukia waovu na wale wanaopenda mapigano.
6Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka; upepo wenye joto kali ndio fungu lao.
7Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, yeye hupenda haki. Wanyofu watauona uso wake.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.