A ruler weighs testimony beside honest market scales as farmers plow and draw from a deep well

Mithali 20

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi; yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.
2Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.
3Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi, bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.
4Mvivu halimi kwa majira; kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama lakini hapati chochote.
5Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina, lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.
6Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma, bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?
7Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama, wamebarikiwa watoto wake baada yake.
8Mfalme anapoketi kwenye kiti chake cha ufalme kuhukumu, hupepeta ubaya wote kwa macho yake.
9Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi; mimi ni safi na sina dhambi?”
10Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti, Mwenyezi Mungu huchukia vyote viwili.
11Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake, kama tabia yake ni safi na adili.
12Masikio yasikiayo na macho yaonayo: Mwenyezi Mungu ndiye alivifanya vyote viwili.
13Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini, uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.
14“Haifai, haifai!” asema mnunuzi, kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.
15Kuna dhahabu, na marijani kwa wingi, lakini midomo inayonena maarifa ni kito cha thamani.
16Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie liwe dhamana kwa ajili ya mgeni.
17Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu, bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.
18Fanya mipango kwa kutafuta mashauri, ukipigana vita, tafuta maelekezo.
19Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika, kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.
20Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake, taa yake itazimwa katika giza nene.
21Urithi upatikanao haraka mwanzoni, hautabarikiwa mwishoni.
22Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!” Mngojee Mwenyezi Mungu, naye atakuokoa.
23Mwenyezi Mungu anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu, nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.
24Hatua za mtu huongozwa na Mwenyezi Mungu. Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?
25Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.
26Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu, hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.
27Taa ya Mwenyezi Mungu huchunguza roho ya mwanadamu, huchunguza utu wake wa ndani.
28Upendo na uaminifu humweka mfalme salama; kiti chake cha ufalme huwa salama kwa upendo.
29Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee.
30Mapigo na majeraha huusafisha ubaya, nayo michapo hutakasa utu wa ndani.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.