Jonah kneels in prayer inside the shadowed great fish as seaweed and deep water surround him and warm light descends from above

Yona 2

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Akiwa ndani ya tumbo la samaki, Yona alimwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wake.
2Akasema: “Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu.
3Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka; mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu.
4Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’
5Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu.
6Nilizama chini sana hata pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu.
7“Uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, Mwenyezi Mungu, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu.
8“Wale watu wanaoshikilia sanamu batili hupoteza neema yao.
9Lakini mimi nitakutolea dhabihu, kwa sauti za shukrani na shangwe. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa Mwenyezi Mungu.”
10Basi Mwenyezi Mungu akamwamuru yule samaki, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.
‹ Yona 1Yona 3 ›

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.