Jeremiah lifting a decayed linen belt from a stream while proud leaders stand outside distant Jerusalem

Yeremia 13

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Hili ndilo Mwenyezi Mungu aliloniambia: “Nenda ununue mkanda wa kitani, ujivike kiunoni mwako, lakini usiuache uguse maji.”
2Kwa hiyo nikanunua mkanda, kama Mwenyezi Mungu alivyoniagiza, nikajivika kiunoni.
3Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kwa mara ya pili:
4“Chukua mkanda ulionunua ambao umeuvaa kiunoni mwako, uende sasa Frati uufiche ndani ya ufa mdogo kwenye mwamba.”
5Ndipo nikaenda na kuuficha ule mkanda huko Frati, kama Mwenyezi Mungu alivyoniamuru.
6Baada ya siku nyingi Mwenyezi Mungu akaniambia, “Nenda sasa Frati ukauchukue ule mkanda niliokuambia uufiche huko.”
7Hivyo nikaenda Frati na kuuchimbua ule mkanda kutoka pale nilipokuwa nimeuficha, lakini sasa ulikuwa umeharibika na haufai tena kabisa.
8Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia:
9“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Vivyo hivyo ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikuu cha Yerusalemu.
10Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wafuatao ukaidi wa mioyo yao na kufuata miungu mingine wakiitumikia na kuiabudu, watakuwa kama mshipi huu ambao haufai kabisa!
11Kwa maana kama vile mshipi ufungwavyo kiunoni mwa mtu, ndivyo nilivyoifunga nyumba yote ya Israeli na nyumba yote ya Yuda,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘ili wawe watu wangu kwa ajili ya utukufu wangu, sifa na heshima yangu. Lakini hawajasikiliza.’
12“Waambie: ‘Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo.’ Wakikuambia, ‘Kwani hatujui kwamba kila kiriba inapasa kijazwe mvinyo?’
13Uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: nitawajaza ulevi wote wanaoishi katika nchi hii, pamoja na wafalme wanaoketi kwenye kiti cha ufalme cha Daudi, makuhani, manabii na wakaaji wote wa Yerusalemu.
14Nitawagombanisha kila mmoja na mwenzake, baba na wana wao, asema Mwenyezi Mungu. Sitawarehemu wala kuwahurumia ili niache kuwaangamiza.’ ”
15Sikieni na mzingatie, msiwe na kiburi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenena.
16Mpeni utukufu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, kabla miguu yenu haijajikwaa juu ya vilima vitakavyotiwa giza. Mlitarajia nuru, lakini ataifanya kuwa giza nene na kuibadili kuwa huzuni kubwa.
17Lakini kama hamtasikiliza, nitalia sirini kwa ajili ya kiburi chenu; macho yangu yatalia kwa uchungu, yakitiririka machozi, kwa sababu kundi la kondoo la Mwenyezi Mungu litachukuliwa mateka.
18Mwambie mfalme na mama malkia, “Shukeni kutoka viti vyenu vya utawala, kwa kuwa taji zenu za utukufu zitaanguka kutoka vichwani mwenu.”
19Miji ya Negebu itafungwa, wala hapatakuwa na mtu wa kuifungua. Watu wa Yuda wote watapelekwa uhamishoni, wakichukuliwa kabisa waende mbali.
20Inua macho yako uone wale wanaokuja kutoka kaskazini. Liko wapi lile kundi ulilokabidhiwa, wale kondoo uliojivunia?
21Utasema nini Mwenyezi Mungu atakapowaweka juu yako wale ulioungana nao kama rafiki zako maalum? Je, hutapatwa na uchungu kama mwanamke aliye katika uchungu wa kuzaa?
22Nawe ukijiuliza, “Kwa nini haya yamenitokea?” Ni kwa sababu ya dhambi zako nyingi marinda yako yameraruliwa na mwili wako umetendewa vibaya.
23Je, Mkushi aweza kubadili ngozi yake au chui kubadili madoadoa yake? Vivyo hivyo, wewe uliyezoea kutenda mabaya huwezi kufanya mema.
24“Nitawatawanya kama makapi yapeperushwayo na upepo wa jangwani.
25Hii ndiyo kura yako, fungu nililokuamulia,” asema Mwenyezi Mungu, “kwa sababu umenisahau mimi na kuamini miungu ya uongo.
26Nitayafunua marinda yako juu ya uso wako ili aibu yako ionekane,
27yaani uzinzi wako na kulia kwako kulikojaa tamaa kama farasi, na ukahaba wako usio na aibu! Nimeyaona matendo yako ya machukizo juu ya vilima na mashambani. Ole wako, ee Yerusalemu! Utaendelea kuwa najisi hadi lini?”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.