An elderly potter shaping clay as repentant families kneel among Jerusalem's broken walls

Isaya 64

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Laiti ungepasua mbingu na kushuka chini, ili milima itetemeke mbele zako!
2Kama vile moto unavyoteketeza vijiti na kusababisha maji kuchemka, shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako, na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako!
3Kwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia, ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako.
4Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia, hakuna sikio lililotambua, hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe, anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.
5Uliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha, wale wazikumbukao njia zako. Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako, ulikasirika. Tutawezaje basi kuokolewa?
6Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi, nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu; sisi sote tunasinyaa kama jani, na kama upepo maovu yetu hutupeperusha.
7Hakuna yeyote anayeliitia jina lako wala anayejitahidi kukushika, kwa kuwa umetuficha uso wako na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu.
8Lakini, Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Baba yetu. Sisi ni udongo, na wewe ndiwe mfinyanzi; sisi sote tu kazi ya mkono wako.
9Ee Mwenyezi Mungu, usikasirike kupita kiasi, usizikumbuke dhambi zetu milele. Ee Bwana, utuangalie, twakuomba, kwa kuwa sisi sote tu watu wako.
10Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa; hata Sayuni ni jangwa, Yerusalemu ni ukiwa.
11Hekalu letu takatifu na tukufu, ambako baba zetu walikusifu wewe, limechomwa kwa moto, navyo vitu vyote tulivyovithamini vimeharibika.
12Ee Mwenyezi Mungu, baada ya haya yote, utajizuia? Je, utanyamaza, na kutuadhibu kupita kiasi?

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.