Isaiah kneeling in a smoke-filled temple as a seraph brings a glowing coal toward him

Isaya 6

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi kwenye kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu.
2Juu yake walikuwa maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka.
3Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni; dunia yote imejaa utukufu wake.”
4Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.
5Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi kati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
6Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni.
7Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”
8Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayeenda kwa ajili yetu?” Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”
9Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa: “ ‘Mtaendelea daima kusikiliza, lakini kamwe hamtaelewa; mtaendelea daima kutazama, lakini kamwe hamtatambua.’
10Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu, fanya masikio yao yasisikie, na upofushe macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, nao wakageuka, wakaponywa.”
11Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?” Naye akanijibu: “Hadi miji iwe imeachwa magofu na bila wakazi, hadi nyumba zitakapobaki bila watu, na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,
12hadi Mwenyezi Mungu atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana, na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.
13Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi, itaharibiwa tena. Lakini kama vile mvinje au mwaloni ubakizavyo visiki unapokatwa, ndivyo mbegu takatifu itakavyokuwa kisiki katika nchi.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.