
Isaya 45
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kwa mpakwa mafuta wake, Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume kutiisha mataifa mbele yake na kuwavua wafalme silaha zao, kufungua milango mbele yake ili malango yasije yakafungwa:
2Nitaenda mbele yako na kusawazisha milima; nitavunjavunja malango ya shaba na kukatakata mapingo ya chuma.
3Nitakupa hazina za gizani, mali iliyofichwa mahali pa siri, ili upate kujua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako.
4Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu, Israeli niliyemchagua, nimekuita wewe kwa jina lako, na kukupa jina la heshima, ingawa wewe hunitambui.
5Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, wala hakuna mwingine, zaidi yangu hakuna Mungu. Nitakutia nguvu, ingawa wewe hujanitambua,
6ili kutoka mawio ya jua hadi machweo yake, watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu wala hakuna mwingine.
7Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza, ninaleta mafanikio na kusababisha maafa. Mimi, Mwenyezi Mungu, huyatenda haya yote.
8“Enyi mbingu juu, nyesheni haki, mawingu na yaidondoshe. Dunia na ifunguke sana, wokovu na uchipuke, haki na ikue pamoja nao. Mimi, Mwenyezi Mungu, ndiye niliyeiumba.
9“Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake, yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi. Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi, ‘Unatengeneza nini wewe?’ Je, kazi yako husema, ‘Hana mikono’?
10Ole wake amwambiaye baba yake, ‘Umezaa nini?’ Au kumwambia mama yake, ‘Umezaa kitu gani?’
11“Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake: Kuhusu mambo yatakayokuja, je, unaniuliza habari za watoto wangu, au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu?
12Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumuumba mwanadamu juu yake. Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu, nikayapanga majeshi yake yote ya angani.
13Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu: nitazinyoosha njia zake zote. Yeye atajenga mji wangu upya, na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni, lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi, asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”
14Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi, nao wale Waseba warefu, watakujia na kuwa wako, watakujia wakijikokota nyuma yako, watakujia wamefungwa minyororo. Watasujudu mbele yako, wakikusihi na kusema, ‘Hakika Mungu yu pamoja nawe, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine.’ ”
15Hakika wewe u Mungu unayejificha, Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli.
16Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika; wataenda kutahayarika pamoja.
17Lakini Israeli ataokolewa na Mwenyezi Mungu kwa wokovu wa milele; kamwe hutaaibika wala kutatahayarika, milele yote.
18Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, yeye aliyeumba mbingu, ndiye Mungu; yeye aliyeifanya dunia na kuiumba, yeye ndiye aliiwekea misingi imara, hakuiumba ili iwe tupu, bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Anasema: “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, wala hakuna mwingine.
19Sijasema sirini, kutoka mahali fulani katika nchi ya giza; sijawaambia wazao wa Yakobo, ‘Nitafuteni bure.’ Mimi, Mwenyezi Mungu, nasema kweli; ninatangaza lililo sahihi.
20“Kusanyikeni pamoja mje, enyi wakimbizi kutoka mataifa. Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili, wale waombao miungu isiyoweza kuokoa.
21Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo; wao na wafanye shauri pamoja. Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani, aliyelitangaza tangu zamani za kale? Je, haikuwa Mimi, Mwenyezi Mungu? Wala hapana Mungu mwingine zaidi yangu mimi, Mungu mwenye haki na Mwokozi; hapana mwingine ila mimi.
22“Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe, enyi miisho yote ya dunia; kwa maana mimi ndimi Mungu, wala hapana mwingine.
23Nimeapa kwa nafsi yangu, kinywa changu kimenena katika uadilifu wote neno ambalo halitatanguka: Kila goti litapigwa mbele zangu, kwangu mimi kila ulimi utaapa.
24Watasema kunihusu, ‘Katika Mwenyezi Mungu peke yake ndiko kuna haki na nguvu.’ ” Wote ambao wamemkasirikia Mungu watamjia yeye, nao watatahayarika.
25Lakini katika Mwenyezi Mungu wazao wote wa Israeli wataonekana wenye haki na watashangilia.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.