Jerusalem's purified remnant gathered beneath a protective canopy of cloud and fire

Isaya 4

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Katika siku ile wanawake saba watamshika mwanaume mmoja wakisema, “Tutakula chakula chetu wenyewe na kuvaa nguo zetu wenyewe, ila wewe uturuhusu tu tuitwe kwa jina lako. Utuondolee aibu yetu!”
2Katika siku ile Tawi la Mwenyezi Mungu litakuwa zuri na lenye utukufu, nalo tunda la nchi litakuwa fahari na utukufu wa wale Waisraeli watakaonusurika.
3Wale watakaoachwa Sayuni, watakaobaki Yerusalemu, wataitwa watakatifu, wale wote ambao wameorodheshwa miongoni mwa walio hai huko Yerusalemu.
4Bwana atausafisha uchafu wa wanawake wa Sayuni, atatakasa madoa ya damu kutoka Yerusalemu kwa Roho ya hukumu na Roho ya moto.
5Kisha Mwenyezi Mungu ataumba juu ya Mlima wote wa Sayuni, na juu ya wale wote wanaokusanyika hapo, wingu la moshi wakati wa mchana, na kung’aa kwa miali ya moto wakati wa usiku; nako juu ya huo utukufu wote kutatanda kifuniko cha ulinzi.
6Utakuwa sitara na kivuli kutokana na joto la mchana, na kuwa mahali pa kujificha kutokana na dhoruba na mvua.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.