People from many nations ascending toward Zion while swords are reshaped into farming tools

Isaya 2

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:
2Katika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Mwenyezi Mungu utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote, utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yatamiminika huko.
3Mataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni kwenye mlima wa Mwenyezi Mungu, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Torati itatoka Sayuni, neno la Mwenyezi Mungu litatoka Yerusalemu.
4Atahukumu kati ya mataifa na ataamua migogoro ya mataifa mengi. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena.
5Njooni, enyi nyumba ya Yakobo, tutembeeni katika nuru ya Mwenyezi Mungu.
6Mwenyezi Mungu umewatelekeza watu wako, nyumba ya Yakobo. Wamejaa ushirikina unaotoka Mashariki, wanapiga ramli kama Wafilisti na wanashikana mikono na wapagani.
7Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hakuna mwisho wa hazina zao. Nchi yao imejaa farasi, hakuna mwisho wa magari yao ya vita.
8Nchi yao imejaa sanamu; wanasujudia kazi za mikono yao, vitu vile vidole vyao vimevitengeneza.
9Kwa hiyo mwanadamu atashushwa na binadamu atanyenyekezwa: usiwasamehe.
10Ingieni kwenye miamba, jificheni ardhini kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake!
11Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa na kiburi cha wanadamu kitashushwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.
12Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anayo siku aliyoiweka akiba kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi, kwa wote wanaojikweza (nao watanyenyekezwa),
13kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana, na mialoni yote ya Bashani,
14kwa milima yote mirefu na vilima vyote vilivyoinuka,
15kwa kila mnara ulio mrefu sana na kila ukuta wenye ngome,
16kwa kila meli ya biashara , na kila mashua ya kifahari.
17Majivuno ya mwanadamu yatashushwa, na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,
18nazo sanamu zitatoweka kabisa.
19Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba, na kwenye mahandaki ardhini kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia.
20Siku ile, watu watawatupia panya na popo sanamu zao za fedha na za dhahabu, walizozitengeneza ili waziabudu.
21Watakimbilia kwenye mapango miambani na kwenye nyufa za miamba kutokana na utisho wa Mwenyezi Mungu na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia.
22Acheni kumtumainia mwanadamu, ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake. Yeye ana thamani gani?

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.