A woman stands where a thorn-blocked barren path opens into a luminous vineyard with grain, oil, water, and peaceful animals

Hosea 2

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1“Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’
2“Mkemeeni mama yenu, mkemeeni, kwa maana yeye si mke wangu, nami si mume wake. Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake na uzinzi kati ya matiti yake.
3Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa. Nitamfanya kama jangwa, nitamgeuza awe nchi ya kiu, nami nitamuua kwa kiu.
4Sitaonesha upendo wangu kwa watoto wake, kwa sababu ni watoto wa uzinzi.
5Mama yao amekosa uaminifu na amewachukua mimba katika aibu. Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu, ambao hunipa chakula changu na maji yangu, sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu na kinywaji changu.’
6Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake kwa vichaka vya miiba, nitamjengea ukuta ili asiweze kutoka.
7Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata; atawatafuta lakini hatawapata. Kisha atasema, ‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza, kwa maana nilikuwa na hali njema kuliko sasa.’
8Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta, niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia kwa kumtumikia Baali.
9“Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari. Nitamnyang’anya sufu yangu na kitani yangu iliyokusudiwa kufunika uchi wake.
10Basi sasa nitaufunua ufisadi wake mbele ya wapenzi wake; hakuna yeyote atakayemtoa mikononi mwangu.
11Nitakomesha furaha na macheko yake yote: sikukuu zake za mwaka, sikukuu za Miandamo ya Mwezi, siku zake za Sabato, sikukuu zake zote zilizoamriwa.
12Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake, ambayo alisema yalikuwa malipo yake kutoka kwa wapenzi wake; nitaifanya kuwa kichaka, nao wanyama pori wataila.
13Nitamwadhibu kwa ajili ya siku alizowafukizia uvumba Mabaali; alipojipamba kwa pete na kwa vito vya thamani, na kuwaendea wapenzi wake, lakini mimi alinisahau,” asema Mwenyezi Mungu.
14“Kwa hiyo sasa nitamshawishi; nitamwongoza hadi jangwani na kuzungumza naye kwa upole.
15Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu, nami nitalifanya Bonde la Akori mlango wa matumaini. Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake, kama siku zile alizotoka Misri.
16“Katika siku ile,” asema Mwenyezi Mungu, “utaniita mimi ‘Mume wangu ’; hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu .’
17Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka mdomoni mwake, wala hataomba tena kwa majina yao.
18Katika siku ile nitafanya agano kwa ajili yao na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani, na viumbe vinavyotambaa ardhini. Upinde, upanga na vita, nitaondolea mbali katika nchi, ili wote waweze kukaa salama.
19Nitakuposa uwe wangu milele; nitakuposa kwa uadilifu na haki, kwa upendo na huruma.
20Nitakuposa kwa uaminifu, nawe utamkubali Mwenyezi Mungu.
21“Katika siku ile nitajibu,” asema Mwenyezi Mungu, “nitajibu kwa anga, nazo anga zitajibu kwa nchi;
22nayo nchi itajibu kwa nafaka, divai mpya na mafuta, navyo vitajibu kwa Yezreeli.
23Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe; nami nitaonesha pendo langu kwake yule ambaye nilimwita, ‘Si Mpendwa Wangu .’ Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio Watu Wangu ,’ ‘Ninyi ni Watu Wangu’; nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu’.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.