
Hosea 14
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Rudi, ee Israeli, kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako. Dhambi zako zimekuwa anguko lako!
2Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Mwenyezi Mungu. Mwambieni: “Samehe dhambi zetu zote na utupokee kwa neema, ili tuweze kutoa matunda yetu kama sadaka za mafahali.
3Ashuru hawezi kutuokoa, hatutapanda farasi wa vita. Kamwe hatutasema tena ‘miungu yetu’ kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza, kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”
4“Nitaponya ukaidi wao na kuwapenda kwa hiari yangu, kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.
5Nitakuwa kama umande kwa Israeli; atachanua kama yungiyungi. Kama mwerezi wa Lebanoni atashusha mizizi yake chini;
6matawi yake yatatanda. Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni, harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.
7Watu wataishi tena kwenye kivuli chake. Atastawi kama nafaka. Atachanua kama mzabibu, nao umaarufu wake utakuwa kama divai inayotoka Lebanoni.
8Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu? Nitamjibu na kumtunza. Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi; kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”
9Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya. Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa. Njia za Mwenyezi Mungu ni adili; wenye haki huenda katika njia hizo, lakini waasi watajikwaa ndani yake.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.