An Israelite father gently teaches a child to walk beside a river settlement as older families follow a road toward the hills

Hosea 11

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1“Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda; nilimwita mwanangu kutoka Misri.
2Lakini kadiri nilivyomwita Israeli, ndivyo walivyoenda mbali nami. Walitoa dhabihu kwa Mabaali na kufukiza uvumba kwa vinyago.
3Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea, nikiwashika mikono; lakini hawakutambua kuwa ni mimi niliyewaponya.
4Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu, kwa vifungo vya upendo; niliondoa nira shingoni mwao nami nikainama kuwalisha.
5“Je, hawatarudi Misri, nayo Ashuru haitawatawala kwa sababu wamekataa kutubu?
6Upanga utavurumishwa katika miji yao, nao utaharibu makomeo ya malango yao na kukomesha mipango yao.
7Watu wangu wamedhamiria kuniacha. Hata wakimwita Yeye Aliye Juu Sana, kwa vyovyote hatawainua.
8“Efraimu, ninawezaje kukuacha? Ee Israeli, ninawezaje kukutoa? Nitawezaje kukutendea kama Adma? Nitawezaje kukufanya kama Seboimu? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zote zimeamshwa.
9Sitatimiza hasira yangu kali, wala sitageuka na kumharibu Efraimu. Kwa kuwa mimi ndimi Mungu, wala si mwanadamu, Aliye Mtakatifu miongoni mwenu. Sitakuja kwa ghadhabu.
10Watamfuata Mwenyezi Mungu; atanguruma kama simba. Anaponguruma, watoto wake watakuja wakitetemeka kutoka magharibi.
11Watakuja wakitetemeka kama ndege wakitoka Misri, kama hua wakitoka Ashuru. Nitawafanya waishi katika nyumba zao,” asema Mwenyezi Mungu.
12Efraimu amenizunguka kwa uongo, nyumba ya Israeli kwa udanganyifu. Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu, hata kinyume cha yule mwaminifu Aliye Mtakatifu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.