Families teaching one another from blank scrolls as sunrise fills a renewed communal home

Waebrania 8

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Aliye Mkuu mbinguni,
2yeye anayehudumu katika patakatifu, hema la kweli lililowekwa na Mwenyezi Mungu, wala si na mwanadamu.
3Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo, ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.
4Kama angekuwa duniani, hangekuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.
5Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Musa alionywa alipokaribia kujenga Maskani, akaambiwa: “Hakikisha kuwa unavitengeneza vitu vyote kwa mfano uliooneshwa kule mlimani.”
6Lakini huduma aliyopewa Isa ni bora kuliko yao, kama vile agano ambalo yeye ni mpatanishi wake lilivyo bora zaidi ya lile la zamani, nalo limewekwa misingi ya ahadi zilizo bora zaidi.
7Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.
8Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema: “Siku zinakuja, asema Mwenyezi Mungu, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.
9Agano langu halitakuwa kama lile nililofanya na baba zao nilipowashika mkono kuwaongoza watoke nchi ya Misri, kwa sababu hawakuendelea kuwa waaminifu katika agano langu, nami nikawaacha, asema Mwenyezi Mungu.
10Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli baada ya siku zile, asema Mwenyezi Mungu. Nitaziweka sheria zangu katika nia zao na kuziandika mioyoni mwao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
11Mtu hatamfundisha tena jirani yake, wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Mwenyezi Mungu,’ kwa sababu wote watanijua mimi, tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana.
12Kwa sababu nitasamehe uovu wao, wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”
13Kwa kuliita agano hili “jipya”, Mungu amefanya lile agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.