Two carpenters examine a charred grapevine branch beside strong cedar beams in a plain workshop

Ezekieli 15

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:
2“Mwanadamu, je, ni vipi mti wa mzabibu unaweza kuwa bora kuliko tawi la mti mwingine wowote ndani ya msitu?
3Je, mti wake kamwe huchukuliwa na kutengeneza chochote cha manufaa? Je, watu hutengeneza vigingi vya kuning’inizia vitu kutokana na huo mti wake?
4Nao baada ya kutiwa motoni kama nishati na moto ukateketeza ncha zote mbili na kuunguza sehemu ya kati, je, unafaa kwa lolote?
5Kama haukufaa kitu chochote ulipokuwa mzima, je, si zaidi sana sasa ambapo hauwezekani kufanyishwa chochote cha kufaa baada ya moto kuuchoma na kuuacha majivu?
6“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kama nilivyoutoa mti wa mzabibu miongoni mwa miti ya msituni kuwa nishati ya moto, hivyo ndivyo nitakavyowatendea watu wanaoishi Yerusalemu.
7Nitaukaza uso wangu dhidi yao. Ingawa watakuwa wameokoka kwenye moto, bado moto utawateketeza. Nitakapoukaza uso wangu dhidi yao, ninyi mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
8Nitaifanya nchi kuwa ukiwa kwa sababu wamekuwa si waaminifu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.