
Mhubiri 11
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Tupa mkate wako juu ya maji, kwa maana baada ya siku nyingi utaupata tena.
2Wape sehemu watu saba, naam hata wanane, kwa maana hujui ni baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
3Kama mawingu yamejaa maji, hunyesha mvua juu ya nchi. Kama mti ukianguka kuelekea kusini au kuelekea kaskazini, mahali ulipoangukia, hapo ndipo utakapolala.
4Yeyote atazamaye upepo hatapanda, yeyote anayeangalia mawingu hatavuna.
5Kama vile usivyofahamu njia ya upepo, au jinsi mwili uumbwavyo ndani ya tumbo la mama, vivyo hivyo huwezi kufahamu kazi ya Mungu, Muumba wa vitu vyote.
6Panda mbegu yako asubuhi, nako jioni usiruhusu mikono yako ilegee, kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa, kwamba ni hii au ni ile, au kwamba zote zitafanikiwa sawasawa.
7Nuru ni tamu, tena inafurahisha macho kuona jua.
8Mtu akiishi miaka mingi kiasi gani, na aifurahie yote. Lakini akumbuke siku za giza, kwa maana zitakuwa nyingi. Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.
9Furahi ewe kijana, ukiwa bado kijana, moyo wako na ukupe furaha siku za ujana wako. Fuata njia za moyo wako na chochote macho yako yanaona, lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote Mungu atakuleta hukumuni.
10Kwa hiyo, ondoa wasiwasi moyoni mwako na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako, kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.