Rich merchants weigh silver beside sandals while a poor laborer is forced into dust near an ignored scroll and compromised altar

Amosi 2

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
1Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Moabu, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu alichoma mifupa ya mfalme wa Edomu, ikawa kama chokaa.
2Nitatuma moto juu ya Moabu ambao utateketeza ngome za Keriothi. Moabu ataanguka kwa ghasia kubwa katikati ya kelele za vita, na sauti ya tarumbeta.
3Nitamwangamiza mtawala wake na kuwaua maafisa wake wote pamoja naye,” asema Mwenyezi Mungu.
4Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Yuda, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Kwa sababu wameikataa Torati ya Mwenyezi Mungu na hawakuzishika amri zake, kwa sababu wamepotoshwa na miungu ya uongo, miungu ambayo babu zao waliifuata.
5Nitatuma moto juu ya Yuda ambao utateketeza ngome za Yerusalemu.”
6Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa dhambi tatu za Israeli, hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu. Wanawauza wenye haki kwa fedha, na maskini kwa jozi ya viatu.
7Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini, kama vile juu ya mavumbi ya nchi, na kukataa haki kwa waliodhulumiwa. Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja, kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu.
8Watu hulala kando ya kila madhabahu juu ya nguo zilizowekwa rehani. Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu.
9“Nilimwangamiza Mwamori mbele yao, ingawa alikuwa mrefu kama mierezi, na mwenye nguvu kama mialoni. Niliyaangamiza matunda yake juu na mizizi yake chini.
10“Niliwapandisha toka Misri, na nikawaongoza miaka arobaini jangwani niwape nchi ya Waamori.
11“Pia niliinua manabii kutoka miongoni mwa wana wenu na Wanadhiri kutoka miongoni mwa vijana wenu. Je, hii si kweli, enyi watu wa Israeli?” asema Mwenyezi Mungu.
12“Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.
13“Sasa basi, nitawaponda kama gari linavyoponda likiwa limejazwa nafaka.
14Mkimbiaji hodari hatanusurika, wenye nguvu wataishiwa nguvu zao, na shujaa hataweza kuokoa maisha yake.
15Mpiga upinde atakimbia, askari wapiga mbio hawataweza kutoroka, na mpanda farasi hataokoa maisha yake.
16Hata askari walio mashujaa sana siku hiyo watakimbia uchi,” asema Mwenyezi Mungu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu — CC BY-SA 4.0. Where these translations come from.

Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Available free at biblica.com and open.bible. Text unchanged, used under CC BY-SA 4.0.